Umoja wa Kiislamu wa Elimu, Uchumi na Maendeleo Zanzibar (UKUEM), umesema unaunga mkono msimamo wa serikali ya Muungano na Zanzibar wa kupinga mashoga na wasagaji kutambuliwa kisheria.
Katibu Mtendaji wa Umoja huo, Sheikh Mohammed Mohammed, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Zanzibar jana, alisema umoja huo unaunga mkono msimamo uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, wa kupinga suala hilo.
Msimamo huo wa serikali unafuatia tishio lililotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Camelon kuzitaka nchi ambazo zinapata misaada kutoka nchi hiyo kuingiza katika Katiba haki za kuwatambua mashoga na mahusiani ya jinsia moja ama sivyo zinaweza kunyimwa misaada hiyo.
Sheikh Mohammed alisema kwamba vitendo vya ndoa za jinsia moja vinakwenda kinyume na mila na utamaduni wa mwafrika pamoja na misingi ya imani za dini hivyo siyo busara kuruhusu kuwepo kwa sheria kama hiyo.
Alisema kwamba matatizo ya kiuchumi isiwe sababu kwa nchi maskini kulazimishwa kufuata sheria zinazo kwenda kinyume na mila na utamaduni wa wananchi wake.
“Bado tunasema kuwa huu ni mwanzo mzuri wa kukabiliana na viongozi wanaotaka kueneza ufisadi kwa kutumia uwezo wao wa kiuchumi kulazimisha mila na silka zao zikubalike hata kama zinakwenda kinyume na mila na utamaduni wa wananchi na imani zao za dini” alisema.
Sheikh Mohammed, alipongeza msimamo ulionyeshwa na viongozi hao na kwamba unapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kwa sababu kuwatambua mashoga ni kwenda kinyume dini, mila na utamaduni wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Aidha, alisema wakati umefika kwa viongozi kuwa makini na mikataba ya kimataifa ili kuepusha sheria zinazotungwa kwenda kinyume na mila na utamaduni na kutoa mfano wa sheria ya haki za watoto iliyopitishwa mwaka huu Zanzibar ilikuwa na kasoro kabla ya kurekebishwa baada ya mzazi kuzuiwa kumchapa bakora mtoto wake.
No comments:
Post a Comment